Rushwa kwenye chaguzi, ufisadi vyamchukiza Sumaye
Na Daniel Mjema,Mwananchi
Posted Jumapili,Decemba29 2013 saa 15:34 PM
Posted Jumapili,Decemba29 2013 saa 15:34 PM
Kwa ufupi
- Sumaye alitoa kauli hiyo jana katika harambee ya kuchangia ujenzi wa ukumbi wa Parokia ya Mawela ya Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi iliyohudhuriwa pia na Mbunge wa Moshi Vijijini, Dk Cyril Chami.
Moshi. Waziri Mkuu Mstaafu,
Frederick Sumaye amesema angefarijika kama wanasiasa wanaojiandaa
kugombea Urais mwaka 2015, wangekemea vitendo vya rushwa na ufisadi
hadharani.
“Zamani uongozi ulikuwa hautafutwi kwa udi na
uvumba wala kwa rushwa, bali anayefaa kuwa kiongozi hutafutwa na jamii
husika kutokana na ubora wake na siyo vishawishi vyake,” alisema Sumaye.
Sumaye alitoa kauli hiyo jana katika harambee ya
kuchangia ujenzi wa ukumbi wa Parokia ya Mawela ya Kanisa Katoliki Jimbo
la Moshi iliyohudhuriwa pia na Mbunge wa Moshi Vijijini, Dk Cyril
Chami.
“Ni ukweli uliowazi kuwa, leo chaguzi zetu
zimegubikwa na rushwa na vishawishi vingi na siyo ubora, uhodari wala
tabia ya anayetaka nafsi hiyo ya uongozi,” alisema Sumaye na kuongeza
kusema:
“Hivi sasa rushwa na matumizi makubwa ya fedha za
kuwanunua wapiga kura vinataka kuwa utaratibu halali wa kuwapata
viongozi wetu kuanzia ngazi za vijiji na mitaa hadi ngazi ya urais.”
Sumaye alisema Tanzania hivi sasa inaingia katika
nyakati za uchaguzi hivyo, inahitaji viongozi watakaowaletea Watanzania
maendeleo ya kweli na kuondokana na umasikini na udhalimu.
“Lakini kama tutakiuka taratibu sahihi za kuwapata
viongozi na badala yake wapiga kura tukanunuliwa kwa kupewa rushwa,
basi tujue tutawapata viongozi wala rushwa,” alisema Sumaye.
“Fadhila zimeanza kuwa nyingi, wapiga kura tayari
wameanza kupigwa mnada na kupangiwa bei kulingana na uhodari au umuhimu
wa nafasi aliyonayo mhusika,” alisisitiza Sumaye.
Sumaye alisema Jamii inapaswa kuyapiga vita mambo
hayo kwa nguvu zote na kusema: “Vita hii ni kali na tusipoangalia sauti
ya wanaopigana inaweza ikafifishwa na kelele za wanaonufaika na rushwa
hizi za nyakati za chaguzi. Inaelekea fedha zinazotumika ni nyingi
sana”.
“Ukikemea tu rushwa basi utapachikwa sababu nyingi
zisizohusika ikiwemo ya kugombea urais mwaka 2015…nasema katika hili,
suala la kugombea au kutogombea urais mwaka 2015 siyo sababu,” alisema.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni